dc.description.abstract | Malengo ya utafiti huu yalikuwa kushughulikia suala la usasa na mwanamke wa kisasa katika
Nyuso za mwanamke. Hii ni riwaya yake S.A Mohammed ya mwaka wa 2010.
Lengo kuu la utafiti lilikuwa kumsawiri mwanamke wa kisasa na jinsi anavyojichukua
kulingana na usasa. Katika hali hiyo tuliweza kusawiri usasa na kuthibitisha kuwa Nyuso za
mwanamke ni riwaya ya kisasa na tukionesha masuala makuu yanayomrejelea mhusika mkuu
aliye kielelezo cha mwanamke wa kisasa. Uhusika wake unadhihirisha mambo mengi
kuhusiana na usasa na vikwazo dhidi ya ufanisi wake kwa mkabala wa usasa. Aidha kuhusika
kwake kunaonekana kama istiara ya mwanamke aliyetambua dhuluma zinazoendelezwa na
jamii na anayepambana kupigania haki za mwanamke. Kupambana kwake ni pamoja na
kuzindua jamii ili itembee na wakati. Hii ina maana ya kuasi utamaduni wenye dhana dufu
zinazoirudisha jamii nyuma.
Pili utendakazi wake unahusu mambo mengi na makubwa ambayo jamii huona vigumu
kutekelezwa na mwanamke. Nadharia iliyotuongoza katika utafiti huu ni ya ufeministi wa
kiafrika. Ilitufaa maana inayo miongozo iliyotuelekeza kujua ni yapi mwanamke wa kiafrika
hupitia na anavyojitahidi kujinasua kutoka kwa dhuluma hizo. Ili kujipa ufahamu zaidi
tuliweza kudurusu tasnifu zilizoshughulikiwa na ambazo zilihusiana na suala letu. Tasnifu
hizo zilisawiri maonevu dhidi ya mwanamke wa kiafrika lakini hazikuangazia ni jinsi gani
mwanamke wa kisasa anavyokabiliana na dhuluma kama hizo na zinazoendelezwa hata
katika jamii ya sasa.
Kuweza kutekeleza wajibu wa utafiti, tumegawa tasnifu hii katika sura tano. Sura ya kwanza
ni kuhusu uteuzi wa mada, madhumuni, msingi wa nadharia na njia za utafiti. Sura ya pili
inayo mukhtasari wa riwaya ya utafiti na vilevile imeshughulikia dhana muhimu ambazo
zimehalalisha usasa unaojitokeza katika riwaya yetu ya utafiti. Sura ya tatu inarejelea
maudhui yanayojikita kwenye utamaduni na yanayokinzana na usasa. Aidha inaonesha
utendakazi ambao unadhibitisha kuwa mhusika mkuu ni mwanamke wa kisasa na aliyeajibika
kulingana na usasa.
Sura ya nne imesawiri ithibati kadhaa zinazoonesha kufaulu kwa mwanamke wa kisasa na
masuala ibuka yanayokwaza ufanisi wake. Kufikia mwisho wa sura hii tunarejelea mikakati
iliyofanikisha ndoto zake na alivyozifuatilia kama suala la kimsingi la kufanikisha utendakazi
wake. Sura ya tano ni ujumla wa matokeo ya yaliyoshughulikiwa na mapendekezo ya yale
yanayoweza kutafitiwa kwa kina ili kukamilisha kwa dhati suala hilo tulilolishughulikia | en |